Powered By Blogger

Monday, July 10, 2017

FAIDA ZA PARACHICHI NA JUISI YAKE

Tupate Elimu Juu PARACHICHI
Parachichi ni tunda ambalo mti wake hujulikana kisayansi kama Persea amerikana.  Tunda hili lina aminika kuwa na asili kutoka jimbo la Puebla, bara Amerika ya kusini kunako nchi ya Mexico. Ushahidi wa kale kabisa, takribani miaka 10000 BC umeonyesha parachichi lilitumika katika jimbo la Puebla nchini Mexico. Lakini kutokana na faida nyingi kiafya zipatikanazo kwa ulaji wa tunda hili, tunda hili sasa hupatikana na kutumika kwa lishe sehemu nyingi duniani hususani barani Afrika.

Parachichi ni tunda la pekee ukilinganisha na matunda mengine, kimsingi matunda mengine huwa yana wanga(carbohydrate) kwa wingi, wakati parachichi lina aina ya mafuta ambayo yana faida kwa afya.

Parachichi katika tafiti nyingi limeonekana kuwa na faida katika afya ya moyo. Wagonjwa wa moyo wamekuwa katika makatazo ya kutumia aina ya mafuta ambayo yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa lehemu katika damu(mafuta hayo kitaalam kama polysaturated fat), na kuongeza matumizi ya mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu (monosaturated fat). Parachichi ni chanzo kizuri cha mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu. Utafiti unaonyesha kuwa matumizi ya mafuta haya  katika parachi hupunguza lehemu iliyo hatari ( kitaalam kama, Low density lipoprotein), na huchangia katika ongezeko la lehemu isiyo hatari( High density lipoprotein).
Madini ya Potasiamu ni aina ambayo huwa watu hawapati ya kutosha kutoka katika vyakula. Parachichi lina kiwango kikubwa cha madini ya potassium kuliko ndizi. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa matumizi ya madini haya huambatana na kupungua kwa shinikizo la damu, shinikizo la juu la damu laweza kupelekea mtu kupata kiharusi, shambulizi la moyo hata figo kushindwa kufanya kazi.

Parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba. Fiba ni kirutubisho kutoka katika vyakula vya jamii ya mimea, fiba huwa hazimeng’enywi tumboni lakini huwa zina umuhimu mkubwa sana, kama kusaidia kupunguza uzito wa mwili, kusaidia urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini na kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengi mwilini. Kuna aina fulani ya fiba ambazo huwa ni virutubisho kwa ajili ya bakteria wenye faida tumboni, hii huimarisha kinga ya mwili na kusaidia mwili kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa. Kwa kuwa parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba, husaidia kuboresha mmeng’enyo na kupata choo katika hali ya kawaida.

Aina ya mafuta na virutubisho tulivyoviona awali katika parachichi vinasaidia afya ya ngozi yako. Husaidia ngozi yako kutokuwa kavu na kuwa na unyevu unaotakiwa na kuifanya ngozi kuwa laini na yenye afya. Vitamini C husaidia katika kusaidia uponaji haraka wa ngozi na kujijenga upya kwa seli za ngozi zilizoharibika,husaidia kujenga elastini na collageni ambazo ni muhimu katika ngozi. Uwepo wa virutubisho viondoavyo sumu(antioxidants) katika parachichi kama carotenoidi na vitamini E, hutusaidia kutukinga na mionzi mikali ya jua, kwa hiyo huzuia makunyanzi katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuwa na mwonekano mzuri wakati wote.

Tunda hili ni lishe bora kwa wale wenye kisukari. Parachichi lina kiwango kidogo cha sukari ukilinganisha na matunda mengine. Pia uwepo wa mafuta aina ya ‘monosaturated’ husaidia kuboresha ufanyaji kazi wa homoni ya insulini, katika urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini. Faida nyingine ni kuwa Vitamini C  katika parachichi husaidia kuimarisha mishipa ya damu na kuboresha kinga ya mwili ambayo ni faida kubwa kwa wagonjwa wenye kisukari.

Faida katika afya ya uzazi ni dhahiri. Parachichi lina Vitamini E ambayo ni “antioxidant”  Potasiamu, Vitamini B6,Vitamini C ambazo hutusaidia kutukinga na magonjwa ya moyo hata yale ya kisukari. Chochote kile kinachosaidia afya ya moyo pia husaidia afya ya uzazi. Wanaume wenye magonjwa ya moyo na kisukari huwa tatizo kubwa la upungufu wa nguvu za kiume.

Parachichi pia limeonekana kuwa na faida nyingi katika kuboresha afya ya macho, viungo vya mwili na nyinginezo nyingi. Katika utafiti mmoja uko Marekani, ulionyesha kuwa watu walao parachichi walionekana kuwa na afya bora ukilinganisha na wale wasiokula parachichi. Waliokula parachichi hawakupatwa  na matatizo ya mmeng’enyo  ukilinganisha na wale wasiokula. Matatizo ya mmeng’enyo huchangia watu kupatwa na magonjwa ya moyo na kisukari.

Hapo ni kwa mafupi tu, Ila kwa ushauri Tuwe tunapendelea kutumia matunda mara kwa mara ili kuweza kupata faida za kiafya na kuboresha miili yetu dhidi ya matatizo madogo madogo ambayo yakikua yanakua ni makubwa na yasiyokua rahisi kuyakabili.
Ukienda sokoni usisahau parachichi aka Avocado.

Waweza ku subscribe katika blog hii ili uwe wa kwanza kupata makala hizi za afya kwa kuingiza email yako..

No comments:

Post a Comment

FEATURED POSTS

AFYA TIPS